Maduka matatu yameteketea kwa moto
katika eneo la Msasani kwa Mwinyi jijini Dar es Salaam na kusababisha
mshutuko mkubwa na taharuki kwa wakazi wa maeneo hayo baada ya kusikika
kwa milipuko ya gesi hali iliyowalazimu wasamaria wema kuamsha majirani
na wenye nyumba kwa kurusha mawe makubwa juu ya mabati ili kuokoa maisha
yao.
ITV ilifika katika eneo la tukio na kushuhudia baadhi ya watu
wakishuhudia moto huo ukijaribu kuzimwa na kikosi cha zima moto, huku
baadhi yao wakisema kwamba baadhi ya watu walipatwa na mshutuko kutokana
na moto huo kusambaa kwa kasi na kulazimu magari manne ya zima moto
kuwasili katika tukio hili kupambana na moto huo.
Mlinzi aliyekuwa katika eneo la maduka hayo, alilazimika kupiga
yowe usiku ili kupata msaada baada ya kupigwa na butwaa na kasi ya moto
huo huku baadhi ya majirani wakisema hali ya tukio la moto huo ilishtua
wengi baada ya kusikika milipuko ya gesi katika moja ya duka iliyokuwa
ikitetea kwa moto na kuongeza kuwa kuchelewa kwa kikosi cha zima moto
ndio iliyosababisha maduka yote matatu kuteketea na kusababisha hasara
ya zaidi ya milioni.
Afisa kutoka kikosi cha zima moto Bwana Saidi Sabauri akiwa katika
eneo la tukio katika jitihada za kuzima moto huo ameeleza jitihada
walizofanya huku mama mwenye nyumba akisema kuwa kutokana na kusumbuliwa
na magonjwa alilazimika kutambaa ili kuokoa maisha yake.
No comments:
Post a Comment