MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk Ali
Mohamed Shein leo anatarajiwa kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuwania
nafasi ya urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM, Ofisi Kuu ya CCM
Kisiwandui mjini hapa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Kamati Maalumu ya
Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi ya CCM Zanzibar Waride Bakari Jabu,
Dk Shein ambaye ni Rais wa Zanzibar atakabidhiwa fomu ya urais na Naibu
Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai.
Waride alisema mara baada ya Dk Shein kukabidhiwa fomu ya kuomba
ridhaa ya kuwania nafasi ya urais kwa tiketi ya CCM, atazungumza na
viongozi wa chama hicho wakiwemo wa wilaya na mikoa ya Unguja na Pemba.
Baadhi ya viongozi ambao atapata nafasi ya kuzungumza nao ni pamoja
na wazee wa chama na waasisi wa mikoa mitatu ya Unguja na Pemba.
DK Shein anakuwa mgombea wa kwanza wa CCM kuchukua fomu kuwania
nafasi ya urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho, ingawa kwa upande
wa upinzani, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Shariff Hamad ambaye pia
ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar ameshachukua fomu.
Wawili hao walichuana katika uchaguzi mkuu uliopita na Dk Shein
kutangazwa mshindi, lakini baadaye iliundwa Serikali ya Umoja wa
Kitaifa.
Taarifa ya chama hicho imesema kwamba hadi sasa hakuna jina la
mwanachama wa CCM aliyetangaza nia ya kutaka kuchukua fomu kuwania
nafasi hiyo ya juu ya uongozi kwa Chama Cha Mapinduzi.
No comments:
Post a Comment