HIVI NDIVYO KITUO CHA POLISI KILIVYOCHOMWA MOTO..

TUKIO la wananchi kuchoma Kituo Kidogo cha Polisi cha Bunju A kilichopo wilayani Kinondoni, jijini Dar mwishoni mwa wiki iliyopita lilizua mshtuko wa aina yake na kuweka rekodi mbaya nchini, Uwazi linakupa habari kamili.
Chanzo cha wananchi hao kuchoma kituo hicho kilielezwa kuwa ni baada ya mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Bunju B aliyetajwa kwa jina la Tabia Omary (11) kugongwa na daladala Julai 10, mwaka huu alipokuwa anavuka kuelekea shuleni.
Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo aliyejitambulisha kwa jina la Miriamu Njuki, katika eneo lililotokea ajali, alikuwepo askari wa usalama barabarani akisaidia watoto hao kuvuka barabara kwa kusimamisha magari lakini dereva huyo wa daladala alikaidi na kumgonga mwanafunzi huyo na kufariki papo hapo.
“Baada ya askari huyo kuona daladala limefanya tukio hilo na kutosimama, ilibidi ajiongeze na kuanza kukimbizana na nalo kwa kutumia gari lingine ambapo alifanikiwa kumkamata dereva huyo,” alisema Miriamu.
Mmoja wa wakazi wa eneo hilo ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema baada ya askari kumkimbiza dereva huyo na kuuacha mwili wa marehemu barabarani kwa muda mrefu ndipo wananchi hao walipopatwa na jazba na kwenda kuchoma moto kituo cha polisi jambo ambalo halikuwa sahihi.
“Hakuna uhusiano wowote kati ya mwanafunzi huyo kugongwa na kuchomwa kituo cha polisi kwa sababu kituo chenyewe kipo umbali mrefu na eneo alipogongewa mwanafunzi huyo, walikuwa na chuki zao tu,” alisema mkazi huyo.
Imeelezwa kuwa wananchi hao baada ya kuchoma moto kituo, wengi wao walikimbilia mikoani kukwepa kukamatwa.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule Msingi Bunju B, Ezekiel Johnson, amesema kukosekana kwa matuta katika eneo hilo kunachangia ajali nyingi kutokea.
“Mpaka sasa wameshagongwa watoto wanne na kati yao, wawili wamepoteza maisha na wawili wamepata ulemavu wa kudumu tangu mwaka huu uanze,” alisema mwalimu huyo.
Katika tukio hilo, wahalifu hao licha ya kupasua vioo na kuiba spea za magari kadhaa yaliyokuwepo kituoni hapo, walifanya uharibifu mkubwa katika gari la mwanamke aliyetambuliwa kwa jina la Husna Shabani
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick aliyekwenda kushuhudia tukio hilo alieleza masikitiko yake kwa wananchi waliochukua sheria mkononi na kumuagiza Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camilius Wambura kuhakikisha watuhumiwa wote wanakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Jeshi la polisi linawashikilia zaidi ya watu 32 kwa tuhuma za kukichoma kituo hicho na upelelezi unaendelea. Marehemu Tabia alizikwa Jumamosi iliyopita katika mtaa wa Chalinze Bunju B ambao ndugu, jamaa na marafiki waliokuwa na simanzi waliangua vilio kwa kuondokewa na mpendwa wao huyo.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved