Shein: Magufuli ndiye kiboko yao

RAIS wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema uteuzi wa mgombea wa CCM katika nafasi ya rais wa Jamhuri ya Muungano katika uchaguzi mkuu, Dk John Magufuli ndio chaguo sahihi la kupambana na upinzani na kuleta ushindi katika CCM na kushika dola.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili Zanzibar kutoka Dodoma, Dk Shein alimtaja Magufuli kama kiongozi hodari muaminifu mwenye shauku kubwa ya kuleta maendeleo ya nchi yake.
Dk Shein katika mkutano mkuu uliomalizika Dodoma hivi karibuni Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi imemwidhinisha kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM tayari kupambana na chama kikuu cha CUF.
Alisema, Magufuli katika nyadhifa mbalimbali alizoshika ameonesha uhodari wa kuchapa kazi na uzalendo pamoja na kusimamia majukumu yake pamoja na walio chini yake. Alifahamisha kwamba ndiyo kigezo sahihi cha kupambana na wapinzani na kuleta maendeleo ya wananchi wa Tanzania.
‘’Mimi namfahamu vizuri sana Magufuli nimefanya kazi naye katika kipindi cha miaka 9 katika baraza la mawaziri nikiwa makamu wa rais......ni mchapa kazi hodari, mwadilifu mwenye mapenzi makubwa na wananchi wake,’’alisema.
Kwa mfano alisema katika Wizara zote alizopata kufanya kazi alionesha uwezo wa ubunifu wa kuleta maendeleo akizitaja Wizara ya Uvuvi pamoja na Ujenzi.
Aidha alimpongeza kwa kumteua Samia Suluhun Hassan, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais kuwa mgombea mwenza huku Chama Cha Mapinduzi kikiweka rekodi ya kuwa na mgombea mwenza mwanamke.
Alisema Samia ameonesha uwezo wa kazi katika nafasi mbalimbali alizopata kuzishika tangu akiwa katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar hadi Muungano.
Alifahamisha kwamba Demokrasia ndani ya Chama Cha Mapinduzi imeimarika kwa kiwango kikubwa ambapo nafasi za wanachama mbalimbali kugombea nafasi za juu za uongozi ni kubwa sana ikiwemo wanawake.
Kwa mfano, alisema Chama Cha Mapinduzi kimeweka historia kubwa ya kuteua wanawake wawili kuingia katika hatua ya mwisho ya uteuzi wa tatu bora. ‘’Hicho ndicho Chama Cha Mapinduzi demokrasia yake katika makundi mbalimbali imekuwa kwa kiwango kikubwa ikiwemo wanawake kushirikishwa katika mchakato wa hatua za mwisho na kushika nafasi ya mgombea mwenza,’’ alisema.
Alipoulizwa kuhusu wingi wa wagombea wa nafasi ya juu ya urais, alisema demokrasia katika Chama Cha Mapinduzi imepanuka kwa kiwango kikubwa tofauti na vyama vyengine vya siasa.
Alisema katika mchakato wa nafasi ya urais jumla ya wanachama wa CCM 42 walijitokeza kuwania nafasi hiyo tofauti na miaka ya 2000 ambapo walijitokeza wanachama 17. ‘’Chama Cha Mapinduzi kinajengwa kwa nguvu ya msingi mmoja mkubwa ambao ni demokrasia iliyopevuka inayotoa makundi mbalimbali ya wanachama kuwania nafasi za juu za uongozi,’’alisema.
Akisoma risala ya wananchi wa mikoa sita kichama, naibu katibu mkuu wa Umoja wa Vijana (UVCCM Zanzibar), Shaka Hamdu alisema wamefurahishwa na maamuzi ya vikao vya chama kuwateuwa wagombea wa nafasi za juu za urais kwa upande wa Jamhuri ya Muungano na Zanzibar.
Shaka alisema wanachama wa CCM Zanzibar wanaunga mkono uteuzi huo wa majina ya viongozi hao ambao watapeperusha bendera ya chama kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu na kukileta ushindi chama.
‘’Wanachama wa mikoa sita matumaini yao makubwa kwamba wagombea wa nafasi za urais kuanzia John Magufuli nafasi ya urais wa Muungano pamoja na Dk Ali Mohamed Shein kwa nafasi ya urais wa Zanzibar kwamba ni uteuzi sahihi wa wagombea wenye sifa watakaokiletea chama ushindi,’’alisema.
Mamia ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi na wananchi kwa ujumla wamejitokeza katika mapokezi ya mgombea wa urais wa Zanzibar kuanzia uwanja wa ndege wa Abeid Amaan Karume hadi katika makao makuu ya CCM Kisiwandui.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved