Kulaaniwa Israel katika Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa

Mabadiliko yanayojiri hii leo duniani yameifanya jamii ya kimataifa kuweza kuzingatia jinai za utawala haramu wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi madhlumu wa Palestina. Kufuatia hali hiyo, jinai za utawala huo hususan jinai ulizozitenda katika vita vya siku 50 dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Ghaza, zimeweza kulaaniwa na jamii ya kimataifa.  Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa limelaani vikali jinai hizo za Israel katika eneo la Ghaza. Taarifa iliyotolewa na baraza hilo la Umoja wa Mataifa hapo jana Ijumaa, baada ya kulipasisha kwa wingi wa kura azimio hilo imelaani jinai za utawala wa Kizayuni za msimu wa joto wa mwaka jana, ambapo maelfu ya raia wasio na hatia wa eneo la Ukanda wa Ghaza waliuawa na maelfu ya wengine kujeruhiwa na kuachwa na vilema vya maisha. Baraza la Haki za Binaadamu pia limetaka kuwajibishwa wahusika wa jinai hizo na kusisitiza kuwa, Israel ilikiuka kwa kiasi kikubwa haki za binaadamu. Ni Marekani pekee ndiyo haikuupigia kwa kura ya ndio muswada huo dhidi ya Israel. Ni vyema kukumbusha kuwa, tarehe nane Julai mwaka jana na ndani ya mwezi wa Ramadhani, utawala wa Kizayuni ulianzisha vita vya siku 50 dhidi ya Ukanda wa Ghaza ambao kwa zaidi ya miaka saba sasa umekuwa chini ya mzingiro wa kila upande kutoka kwa Israel. Katika vita hivyo zaidi ya watu 2,000 wakiwemo mamia ya watoto na wanawake waliuawa shahidi huku wengine karibu elfu 11 wakiwamo watoto 3,000 wakijeruhiwa. Inaelezwa kuwa, tarehe 22 Juni mwaka huu, kamati ya kujitegemea ya uchunguzi iliyo chini ya Umoja wa Mataifa, ilitoa taarifa kuhusiana na jinai za Tel Aviv katika vita hivyo vya siku 50 eneo la Ghaza, ambapo ilisisitiza kuwa Israel ilitekeleza jinai za kivita katika vita hivyo. Jambo lisilo na shaka ni kwamba, hatua ya utawala ghasibu wa Kizayuni katika kutenda jinai za kutisha dhidi ya Wapalestina, kunaiweka wazi asili ya utawala huo mtenda jinai dhidi ya binaadamu na kizazi. Kwa hakika ukali wa jinai zilizotendwa na Israel katika miaka ya hivi karibuni ikiwemo mashambulizi yake dhidi ya Ghaza, umezijeruhi nyoyo za walimwengu. Jinai hizo zimekuwa kubwa kiasi cha kuzifanya asasi za haki za binaadamu duniani likiwemo baraza na taasisi zinazojihusisha katika uwanja huo, kuanzisha uchunguzi wao miezi ya hivi karibuni kwa lengo la kubaini ukubwa wa jinai hizo. Kwa hakika mienendo ya utawala wa Kizayuni inabainisha kuwa utawala huo hauna ukomo wala mpaka katika kutenda jinai zake hizo. Aidha utawala huo, unapata kiburi cha kuendelea na vitendo hivyo kutokana na uungaji mkono wa Wamagharibi juu yake. Kufanywa vikao tofauti na jamii za kimataifa kwa ajili ya kuchunguza jinai za utawala wa Kizayuni na pia kutolewa maazimio na ripoti za Umoja wa Mataifa na asasi za haki za binaadamu zilizo chini ya umoja huo dhidi ya Israel, kunabainisha kwamba sasa walimwengu wameamua kusimama kukabiliana na utawala huo mtenda jinai. Katika mazingira hayo, fikra za walio wengi na raia wa Palestina wanasubiri kuuona Umoja wa Mataifa na asasi zake zinachukua hatua kali na za maana dhidi ya utawala huo ghasibu ili kuionyesha jamii ya kimataifa kuwa asasi hizo kweli zinapambana na dhulma zinazofanywa na Wazayuni dhidi ya raia madhlumu wa Palestina.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved