Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema
hatua zilizochukuliwa mwaka jana na Jamhuri ya Congo Brazaville katika
fremu ya kuwafukuza wahamiaji haramu nchini humo ni kielelezo cha jinai
dhidi ya binadamu. Mwaka 2014 Jamhuri ya Congo Brazaville iliwafukuza
maelfu ya raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mjini Brazaville.
Ripoti
ya Amnesty international imesajili kesi nyingi za ukatili, vitendo vya
utumiaji mabavu na kutiwa nguvuni bila sababu kulikofanywa na vyombo vya
dola vya Jamhuri ya Congo wakati wa kuwafukuza wahamiaji haramu nchini
humo bila ya sababu yoyote. Ripoti hiyo inasema, jinai dhidi ya binadamu
zilifanyika huko Congo Brazaville kwa kisingizio cha kuwasaka na
kuwakamata wahajiri haramu. Katika operesheni hiyo iliyofanyika katika
kipindi cha kati ya Aprili na Septemba 2014, karibu watu laki mbili na
nusu ama walifukuzwa kutoka Congo Brazaville au walilazimika kuondoka
nchini humo. Watu hao waliofukuzwa ni pamoja na wakimbizi waliokwenda
Brazaville wakitafuta kazi na maisha baada ya kukimbia mapigano na
ghasia za mashariki mwa Congo DR. Operesheni hiyo ya kuwafukuza raia wa
DRC kutoka Jamhuri ya Congo ilivuruga uhusiano wa nchi hizo mbili
zinazotenganishwa na Mto Congo.
Wataalamu wa Amnesty International
wanaamini kuwa, operesheni ya kuwafukuza raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Congo kutoka Brazaville ilifanyika kwa shabaha ya kuchochea hisia za
kuwachukia na kuwapiga vita wageni (Xenophobia) nchini humo. Vilevile
maafisa usalama na polisi ya Congo Brazaville waliwanyanyasa kijinsia na
kuwabaka wanawake na wasichana katika operesheni hiyo.
Uchunguzi
uliofanywa na Amnesty International unaonesha kuwa, polisi ya Brazaville
ilitumia vyombo vya mawasiliano ya umma kwa ajili ya kuchochea hisia za
kuwapiga vita na kuwachukia wageni. Uchunguzi huo unaonesha kuwa,
wakati huo zilitungwa nyimbo ambazo zilihamasisha ubaguzi kwa msingi wa
utaifa, jinsia au dini. Nyimbo hizo zilisisitiza kuwa wageni-
wakikusudiwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo- wanapaswa
kurejeshwa nchini kwao.
Kwa sasa Amnesty International imeitaka
serikali ya Congo Brazaville kusitisha mipango na ratiba zote za
serikali ya Brazaville za kuwafukuza nchini humo raia wa kigeni.
Vilevile imeitaka serikali ya Brazaville kuwachukulia hatua za kisheria
wale wote waliohusika na jinai za ukiukaji wa haki za kimataifa za
binadamu.
No comments:
Post a Comment