Sarafraz: Saudi Arabia haijafikia malengo yake Yemen
Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema
kuwa mashambulizi ya miezi mitatu iliyopita ya Saudi Arabia huko Yemen
hayajakuwa na matunda yoyote kwa nchi hiyo. Dakta Muhammad Sarafraz Mkuu
wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria
kushindwa na kugonga mwamba Saudi Arabia huko Yemen na kueleza kuwa:
Licha ya mashambulizi hayo makubwa huko Yemen, lakini Riyadh haijaweza
kutimiza malengo yake ya kijeshi na kisiasa nchini humo na hivi sasa
harakati ya wananchi wa Ansarullah inadhibiti maeneo mengi ya Yemen.
Dakta Sarafraz ameyasema hayo jana katika marasimu ya kuadhimisha mwaka
wa nane tangu kuanzishwa kanali ya matangazo ya Press Tv. Katika sehemu
nyingine ya hotuba yake, Dakta Muhammad Sarafraz ameelezea hali nyeti ya
sasa katika eneo , mazungumzo ya nyuklia ya Iran na kundi la 5+1 na
matukio ya kisiasa ya Uturuki na kuongeza kuwa: Kwa kuzingatia
mabadiliko ya kisiasa yanayojiri nchini Uturuki, upo uwezekano kwa
serikali ya nchi hiyo kuchukua hatua za kichokozi dhidi ya Syria kwa
kustafidi na pengo la madaraka lilipopo nchini humo. Mkuu wa Shirika la
Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia amesema kuwa, kuwepo anga
nzuri ya maelewano na ushirikiano mzuri kati ya wafanyakazi na
wakurugenzi wa kanali ya Press Tv kumekifanya chombo hicho kipate
mafanikio. Katika marasimu hayo ya kuadhimisha mwaka wa nane tangu
kuasisiwa kanali ya Press Tv, naye Muhammad Akhgari Mkurugenzi wa
Kitengo cha Matangazo ya Ng'ambo katika Shirika la Utangazaji la Iran
ameashiria mipango iliyozaa matunda katika kanali ya Press Tv katika
miezi ya hivi karibuni ikiwemo tovuti mpya ya kanali hiyo, na kueleza
kuwa, kanali hiyo ni moja ya mafanikio makubwa ya shirika la utangazaji
la taifa la Iran. Muhammad Akhgari amesema anataraji kuwa mafanikio hayo
yatadumishwa zaidi na zaidi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment