BUNGE limepitisha miswada miwili iliyokuwa imesalia ya mafuta na gesi
ambapo watakaobainika kuchota fedha katika Mfuko wa Mafuta na Gesi
utakaoanzishwa watapewa adhabu mbalimbali ikiwemo kifungo cha miaka 30
jela au kufilisiwa mali zao.
Hata hivyo, wabunge wa upinzani wamemtaka Rais Jakaya Kikwete
wakimuomba asisaini miswada hiyo, huku pia wakitangaza kususia vikao
vyote vilivyobaki vya Mkutano wa 20 wa Bunge, ambalo linatarajiwa
kumaliza uhai wake Alhamisi wiki hii kwa Rais Kikwete kuhutubia.
Akizungumza bungeni jana wakati akifanya majumuisho kwa kujibu hoja
za wabunge mbalimbali waliochangia Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa
Mapato ya Mafuta na Gesi wa Mwaka 2015, Naibu Waziri wa Fedha, Adam
Malima alisema muswada umeweka adhabu kali kwa watakaobainika kutumia
fedha za mfuko huo.
Alizitaja adhabu hizo kuwa ni faini isiyopungua kiasi ambacho mhusika
amechukua, au kifungo cha miaka 30 jela au vyote viwili kwa pamoja na
kuongeza kuwa pia sheria inampa hakimu uwezo wa kutoa adhabu ya
kumfilisi mhusika na kesi hiyo itakuwa ya uhujumu uchumi.
Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Mapato ya Mafuta na Gesi wa Mwaka
2015, unaweka masharti kuhusu uanzishwaji wa Mfuko wa Mafuta na Gesi
ambao utakuwa na Akaunti mbili zitakazotunzwa na kusimamiwa na Benki Kuu
ya Tanzania.
Akaunti hizo ni Akaunti ya Kupokea Mapato na Akaunti ya Kutunza
Mapato. Muswada mwingine uliopitishwa jana ni Muswada wa Sheria ya Uwazi
na Uwajibikaji katika Tasnia ya Uchimbaji Tanzania wa Mwaka 2015,
ambapo wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge waliochangia, Waziri wa
Nishati na Madini, George Simbachawene, alisema unalenga kuondoa
changamoto mbalimbali zilizojitokeza kwenye sera, sheria na miongozo
mbalimbali ambayo ilikuwepo kwa muda mrefu ili kuleta ufanisi bora zaidi
katika sekta ya gesi asilia.
Pamoja na mambo mengine, muswada huo unaanzisha taasisi tatu mpya
ambazo ni Ofisi ya Ushauri Kuhusu Petroli na Gesi chini ya Ofisi ya
Rais, Kampuni ya Mafuta ya Taifa na Mamlaka ya Udhibiti wa Shughuli za
Mkondo wa Juu wa Mafuta (PURA). Pia unaweka uwazi katika leseni na
mikataba ya madini, gesi na mafuta.
Muswada huo ulipitishwa na wabunge wengi wa CCM, huku wa upinzani
wakiwa wanne tu, ambao ni Philipa Mturano na Leticia Nyerere (Viti
Maalumu Chadema) na wawili wa CUF, Said Suleiman Said (Mtambwe) na Hamad
Rashid Mohammed (Wawi).
Akizungumza baada ya Bunge kupitisha miswada hiyo kwa nyakati tofauti
jana, Spika wa Bunge, aliwapongeza wabunge kwa michango yao katika
kuiboresha na kwamba sasa wanasubiri Rais Kikwete aisaini iwe sheria.
Muswada wa Sheria ya Petroli wa Mwaka 2015 wenyewe ulipitishwa juzi.
Wakati huohuo, akizungumza na waandishi wa habari hotelini mjini hapa
jana, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzania Bungeni, Freeman Mbowe,
alisema wanaomba Rais Kikwete asisaini miswada hiyo, ambayo
iliwasilishwa kwa pamoja bungeni Jumamosi.
Pia alisema wabunge wote wa upinzani hawatahudhuria vikao vyote
vilivyobaki vya Bunge ikiwa ni pamoja na kile cha Alhamisi, ambapo Rais
Kikwete atahutubia Bunge ikiwa ni hatua mojawapo ya kuhitimisha uhai wa
miaka mitano wa bunge hilo.
Alisema wabunge wote hao ambao wanatoka vyama vya Chadema, CUF,
NCCR-Mageuzi NLD vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
walitarajiwa kuondoka Dodoma jana kurejea Dar es Salaam kwa ajili ya
vikao zaidi kwenye vyama vyao na baada ya kesho watazungumza hatua
itakayofuata.
No comments:
Post a Comment