Yanga yageukia Polisi

MABINGWA wa soka wa Tanzania Bara, Yanga watacheza na Kombaini ya Polisi Tanzania katika mechi ya kirafiki itakayofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Jumamosi wiki hii.
Mechi hiyo ni kwa ajili ya kujiweka sawa kwa mashindano yanayozikabili timu hizo mbili ambapo Yanga inajiandaa kushiriki Kombe la Kagame litakaloanza Dar es Salaam, Julai 18, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi jana kwa vyombo vya habari, Kombaini ya Polisi itashiriki katika michezo ya Umoja wa Wakuu wa Majeshi ya Polisi Kusini mwa Afrika (SARPCCO) itakayoanza mwishoni mwa mwezi huu nchini Swaziland.
Akizungumza jana Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Michezo wa Jeshi la Polisi, Jonas Mahanga alisema kikosi cha Polisi kitatumia mchezo huo kubaini upungufu na kuufanyia marekebisho kabla ya kuelekea Swaziland ambapo alisema taratibu zote zimeshakamilika.
Mahanga alisema mchezo huo utakuwa mzuri na wa kuvutia kutokana na wachezaji wanaounda Kombaini ya Polisi kuonesha kiwango kikubwa katika kambi yao inayoendelea katika Chuo cha Taaluma ya Polisi (DPA) kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaam.
Alisema Kombaini ya Polisi inaundwa na wachezaji askari kutoka timu za Polisi za Tanzania Bara na Zanzibar ambapo wengi wa wachezaji hao ni wale waliokuwa wanacheza Ligi Kuu zao pamoja na Ligi Daraja la Kwanza.
Aidha, Mahanga alisema kwa upande wa netiboli, nayo itacheza mchezo wa kirafiki na Kombaini ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania ili kuhakikisha kuwa inafanya vizuri nchini Swaziland na kurudi na ubingwa.
Alisema kwa ujumla timu zote zinazojiandaa na michezo hiyo zinaendelea vizuri ambapo wanariadha waliokuwa katika kambi ya Taifa mkoani Manyara wiki hii wataungana na wenzao ili kufanya mazoezi kwa pamoja.
Alisema lengo la michezo hiyo ya SARPCCO ni kujenga mahusiano miongoni mwa askari Polisi wa nchi za kusini mwa Afrika pamoja na kubadilishana mbinu za kukabiliana na uhalifu ambapo Polisi Tanzania itashiriki katika mchezo wa mpira wa miguu, netiboli, riadha na vishale.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved