Magufuli leo mguu sawa kwa urais

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli leo anatarajiwa kuchukua fomu ya uteuzi katika Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili kusaka wadhamini na kisha kuidhinishwa kuwa mgombea katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.
Waziri huyo wa Ujenzi anatarajiwa kuchukua fomu saa sita kamili mchana, na kwa mujibu wa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Nape Nnauye, mgombea huyo atafuatana na mgombea mwenza, Samia Suluhu Hassan na viongozi waandamizi wa chama hicho tawala. Nape aliwaambia waandishi wa habari jana katika Ofisi Ndogo ya CCM, Mtaa wa Lumumba Dar es Salaam kuwa Dk Magufuli na msafara wake, wataondoka katika ofisi hizo saa tano asubuhi kwenda Ofisi za NEC zilizoko Mtaa wa Garden katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
“Mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli atachukua fomu kesho (leo) saa sita mchana. Msafara wake utaondoka hapa (Ofisi Ndogo) saa tano kamili na ataambatana na mgombea mwenza na viongozi waandamizi akiwamo Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Katibu Mkuu, wajumbe wa Sekretarieti, Kamati za Siasa za Wilaya na Mkoa wa Dar es Salaam,” alieleza Nape.
Aliongeza kuwa msafara huo, utapitia katika barabara za Morogoro, Bibi Titi Mohammed na Ohio, na kurudi kwa njia hizo hadi Ofisi Ndogo Lumumba ambako Dk Magufuli atatoa neno la shukrani kwa wanachama, mashabiki na wapenzi wa chama hicho kikongwe na tawala nchini, na Watanzania kwa ujumla.
“Dk Magufuli akishachukua fomu atarejea hapa Ofisi Ndogo na kutoa neno la shukrani kwa kuzungumza na Watanzania wataokuwapo, wanachama na mashabiki wetu ifikapo saa saba mchana,” alieleza Nape ambaye mwishoni mwa wiki aliongoza katika kura za maoni za ubunge katika Jimbo la Mtama mkoani Lindi.
Dk Magufuli alishinda uteuzi wa kuwa Mgombea Urais wa CCM katika vikao vyake vilivyofanyika mjini Dodoma mapema mwezi uliopita, akiwashinda wenzake 38 ambao walikuwa miongoni mwa 42 waliochukua fomu.
Alikuwa miongoni mwa wagombea watano waliopitishwa na Kamati Kuu na kisha kupigiwa kura na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM akiwa na Dk Asha-Rose Migiro, Balozi Amina Salum Ali, January Makamba na Bernard Membe, ambapo yeye, Dk Migiro na Balozi Amina walishinda kwenda kupigiwa kura katika Mkutano Mkuu.
Katika Mkutano Mkuu Maalumu uliofanyika kwa siku mbili kuanzia Julai 11, mwaka huu, Dk Magufuli aliwashinda wanawake hao wawili na kupewa jukumu la kupeperusha bendera ya CCM Oktoba 25, dhidi ya vyama vingine.
Historia yake John Pombe Joseph Magufuli alizaliwa tarehe 29 Oktoba 1959 wilayani Chato mkoani Kagera (sasa mkoa mpya wa Geita). Magufuli alianza elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Chato wilayani Chato mwaka 1967 na alihitimu mwaka 1974.
Alijiunga na Shule ya Seminari Katoke wilayani Biharamulo, ambako alisoma kidato cha kwanza na cha pili mwaka 1975 – 1977. Alihamishiwa Shule ya Sekondari Lake mkoani Mwanza, ambako alisoma kidato cha tatu na nne mwaka 1977 - 1978.
Masomo ya kidato cha tano na sita aliyapata mkoani Iringa katika Shule ya Sekondari Mkwawa kati ya mwaka 1979 na 1981. Alirudi Chuo cha Ualimu Mkwawa kusomea Stashahada ya Elimu ya Sayansi katika masomo ya Kemia, Hisabati na Elimu.
Alisoma hapo mwaka 1981 – 1982. Baada ya kuhitimu hapo, alianza kazi ya ualimu katika Shule ya Sekondari Sengerema mkoani Geita, akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati kati ya mwaka 1982 na 1983.
Baadaye alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika kwa mujibu wa sheria akianzia Makutupora, Dodoma (Julai - Desemba 1983), kisha kambi ya Makuyuni, Arusha (Januari hadi Machi 1984) na akamalizia kambi ya Mpwapwa mkoani Dodoma (Machi – Juni 1984).
Mwaka 1985 alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akisomea Shahada ya Sayansi ya Elimu akibobea kwenye masomo ya Kemia na Hisabati na alihitimu mwaka 1988. Mwaka 1989 - 1995 alifanya kazi katika kiwanda cha Nyanza Cooperative Union (Ltd.) akiwa mkemia na wakati huohuo alianza masomo ya Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Chuo Kikuu cha Salford nchini Uingereza, kikishirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alisoma kati ya mwaka 1991 na 1994.
Magufuli aliendelea na elimu ya juu zaidi kwa maana ya Shahada ya Uzamivu ya Kemia kuanzia mwaka 2000 hadi 2009, ambayo aliihitimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuwa mhitimu wa shahada ya udaktari. Dk Magufuli ana mke na watoto kadhaa.
Dk Magufuli alichaguliwa kuwa mbunge wa Chato mwaka 1995, na aliposhinda Rais Benjamin Mkapa alimteua kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Miundombinu. Katika uchaguzi wa mwaka 2000, Dk Magufuli aligombea na kushinda kwa mara ya pili.
Rais Mkapa alimteua kuwa Waziri wa Wizara ya Miundombinu . Mwaka 2005 alichaguliwa kuwa mbunge kwa kipindi cha tatu na Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hadi mwaka 2008, alipohamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambayo aliiongoza hadi mwaka 2010.
Mwaka 2010 alifanikiwa kuchaguliwa kuwa mbunge kwa mara ya nne na Rais Kikwete alimrudisha katika Wizara ya Ujenzi, ambako yupo hadi hivi sasa.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved