WAKRISTO WA ITALIA WAWEZESHA ZAHANATI YA KISASA VIKAWE




IMG_0282
Mkuu wa Masista Waabuduo Damu ya Kristo, Euprasia Julius akimtambulisha mgeni rasmi na meza kuu kwa wageni waalikwa na wanakijiji wa Vikawe (hawapo pichani) katika hafla ya ufunguzi wa Zahanati ya Da.Ma Africa Maria De Mathias (MDM) Vikawe, Kibaha.
MGANGA Mkuu wa halmashauri ya Mji Kibaha, Dk. Happniness Ndosi amepongeza shirika la masisita wa Waabuduo Damu ya Kristo kwa kufanikisha ujenzi wa zahanati ya kisasa katika kijiji cha Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani.
Mganga huyo ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa zahanati hiyo,pamoja na kuwapongeza amesema serikali itaendelea kushirikiana na mashirika yote kwa lengo la kuwezesha kila kijiji kiwe na zahanati na kila kata kituo na kila wilaya kuwa na hospitali.
Aliwapongeza masista hao kwa kuonesha upendo na huruma kama Biblia inavyomsimulia msamaria mwema ambaye alikuta mtu aliyepigwa na majambazi na kumsaidia.
Aliahidi ushirikiano wa serikali katika kufanikisha usajili wa zahanati hiyo na kuendelea kuisaidia hatua kwa hatua hadi inakuwa kituo mpaka watakapofanikisha safari yao ya kuwa hospitali kubwa ya kisasa.
Mganga huyo pamoja na kutoa ahadi hiyo aliwataka wananchi wa Vikawe kutumia huduma hiyo na kwamba zahanati hiyo itakapohitaji msaada wa gari la kubebea wagonjwa (Ambulance) wataletewa kuchukua mgonjwa na kumfikisha panapohusika.
Zahanati hiyo ya DA.MA Africa imejengwa kwa ufadhili wa wakristo wa Italia chini ya usimamizi wa Muitalia, Germano Frioni.
Akitoa salamu zake Muitalia huyo amesema kwamba anawashukuru wakazi wa Vikawe kwa kumpa nguvu ya kusonga mbele hasa kwa kutambua kwamba yeye na marafiki zake wamefanyakazi usiku na mchana kutafuta fedha kwa ajili ya kusaidia marafiki wa Afrika.
Alisema atajitahidi kufanya kila linalowezekana kuhakikisha changamoto za zahanati hiyo zinafanyiwa kazi.(VICTOR)

Aliwaomba wananchi wa Tanzania kuendelea kumuombea yeye na wenzake kama Papa Francis anavyoagiza ili malengo ya safari ya kuwapo duniani yafanikiwe.
Alisema kwamba watoto wake Daniel na Marco (kwa sasa wote ni marehemu) ambao ndio kifupi cha zahanati hiyo DA.MA wamemfanya kujitambua na kusaidia wengine katika kuonesha upendo.
Aidha alisema kwamba ataendelea kukumbuka Vikawe kwani alifika mara ya kwanza mwaka 2005 na kuona hali ilivyokuwa ambapo sasa lipo jengo la zahanati hiyo likiwa limekamilika.
Wazo la ujenzi wa zahanati hiyo , lilitolewa na wananchi wa Vikawe kwa Masisita Waabuduo Damu ya Kristo mwaka 2004 wakati wakiwa katika eneo hilo baada ya kununua ekari 40 kwa ajili ya kilimo mwaka 1994.
Alisema pamoja na maombi hayo na wao wenyewe kutambua kwamba kuna mahitaji makubwa ya huduma ya afya japokuwa kuna zahanati ya serikali, hawakuweza kutekeleza maombi ya wanavijiji hadi mwaka 2011 walipofanikiwa kupata ufadhili kutoka Italia na kuanza ujenzi mwaka 2013.
Katika risala yao walisema kwa ushirikiano kati yao na wafadhili hao wamefanikiwa kuwapo kwa zahanati hiyo yenye mahitaji yote ya msingi kwa mujibu wa taratibu za serikali na kuzidi.
Msoma risala alisema kwamba wataendelea kupanua miundombinu mpaka zahanati hiyo ifikie ngazi ya cha afya na baadae hospitali.
Pamoja na ujenzi wa zahanati hiyo ya kisasa masisita hao wameanzisha shule ya awali kuwaandaa wanafunzi wa darasa la kwanza.
Wamesema kwamba wanaamini kwamba wataendelea kushirikiana na wananchi na wadau wengine wa afya katika kuimarisha huduma za hospitali hiyo.
Zahanati hiyo pamoja na vifaa tiba pia ina raslimali ya visima vya maji ya mvua ujazo zenye ujazo wa lita laki moja na kingine lita 49 elfu, wanatumia umeme wa sola na jenereta .
Walisema kwamba wanachangamoto ya kukosa umeme wa Tanesco, barabara nzuri na nyumba za wafanyakazi.

No comments:

Post a Comment

©2015 New Day Pro Media.All Rights Reserved